WAFANYIKAZI KAUNTI YA TRANS NZOIA WAHIMIZWA KUSHIRIKIANA KIKAMILIFU NA SERIKALI.

Chama cha kutetea maslahi ya wafanyikazi katika kaunti ya Trans nzoia kimewahimiza wafanyikazi wa kaunti hiyo kushirikiana kikamilifu na uongozi wa gavana George Natembeya katika juhudi za kuimarisha miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.

Mwenyekiti wa chama hicho Samwel Kiboi aliwataka wafanyikazi wa kaunti hiyo kujihusisha zaidi na utendakazi wao wa kutoa huduma kwa wananchi akielezea imani kwamba mazingira ya wafanyikazi yataimarishwa chini ya utawala wa Gavana Natembeya kinyume na ilivyokuwa katika serikali iliyotangulia.

“Kwa miaka kumi iliyopita wafanyikazi walipitia hali ngumu sana, ila sasa nafahamu kwamba wataweza kupata afueni chini ya serikali ya sasa. Mimi nataka kuwaomba wafanyikazi kushirikiana kikamilifu na serikali ili kuhakikisha kwamba gavana wa kaunti hii anafanikisha ajenda zake kwa mwananchi.” Alisema Kiboi.

Wakati uo huo Kiboi aliwataka wafanyikazi kujiepusha na swala la kuegemea mirengo ya kisiasa na badala yake kutumia muda wao mwingi kuwahudumia wananchi, akiwakumbusha kwamba kipindi cha siasa kilikamilika na uchaguzi wa mwezi agosti.

“Tunafaa kujitenga na miegemeo ya kisiasa na badala yake kuangazia zaidi huduma kwa wananchi. Uchaguzi ulikamilika mwezi agosti na sasa ni wakati ambapo wananchi wanafaa kupata huduma bora kutoka kwa wafanyikazi wote wa kaunti.” Alisema Kiboi.