WAFANYIBIASHARA KONGELAI WALALAMIKIA HALI MBOVU YA SOKO HILO.


Wafanyibiashara katika soko la Kongelai eneo la Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia hali mbovu ya soko hilo huku wakitoa wito kwa serikali ya kaunti hii kuboresha hali ya soko hilo.
Wakiongozwa na Rosana Kashiol wafanyibiashara hao wamesema kuwa soko hilo lina choo kimoja tu na ambacho hufunguliwa siku ya soko pekee huku kikisalia kufungwa siku zingine maji pia yakiwa tatizo katika soko hilo.
Aidha wafanyibiashara hao wamelalamikia kutokuwa na sehemu ya kujizuia na jua kali au wakati inaponyesha mvua huku bidhaa zao zikiharibiwa kwa kunyeshewa na mvua wakimtaka gavana wa kaunti hii kuingilia kati na kuhakikisha soko hilo linashughulikiwa ili kutoa mazingira bora ya kutekelezea shughuli zao.
Wakati uo huo wahudumu wa boda boda eneo hilo wamelalamikia hali mbovu ya barabara huku wito ukitolewa kwa wadau kuhakikisha wahudumu hao wanapewa mafunzo kuhusu sheria za barabarani.