WADAU WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILI MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA MIONGONI MWA VIJANA KACHELIBA.

Ipo haja kwa wadau mbali mbali kaunti ya Pokot magharibi kujitokeza na kubuni mikakati ya kukabiliana na matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana.

Ni wito wake askofu wa kanisa la AIC kaunti hiyo David Kaseton ambaye alisema kwamba wengi wa vijana hasa wa kiume wamejiingiza katika matumizi ya mihadarati kufuatia shinikizo kutoka kwa vijana wengine hasa wakiwa katika shule za upilli na vyuo vikuu, ambapo wanakutana na wanafunzi kutoka maeneo mengine ya nchi.

Aidha Kaseton alitaja misingi ya malezi kuwa chanzo cha vijana wengi katika jamii kujihusisha na matumizi ya mihadarati.

“Shinikizo kutoka kwa vijana wengine hasa katika shule za upili au vyuo vikuu ambapo wanakutana na wanafunzi kutoka meneo mbali mbali ambao pia wamelelewa katika misingi tofauti, zimepelekea vijana wengi katika kaunti hii ya Pokot magharibi kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.” Alisema Kasaton.

Kaseton alisema kwamba kama kanisa wameanzisha mipango mbali mbali ya kuwasaidia vijana kujitenga na matumizi ya mihadarati ikiwemo kuwatumia wakazi mbali mbali wa kaunti hii waliofaulu maishani pamoja na wataalam kuwashauri vijana hawa kuhusu umuhimu wa kujitenga na hulka hiyo.

“Katika kila likizo huwa tunaandaa mikutano ili kuwaongelesha vijana, ambapo tunawaleta wataalam tofauti  kuwahimiza kuhusu umuhimu wa kujitenga na matumizi ya dawa za kulevya. Pia tuna wakazi wa kaunti hii ambao wamefaulu katika Nyanja mbali mbali ambao pia tunawatumia katika kuwaongelesha vijana wetu.” Alisema.