WADAU WATAKIWA KUWASHAURI VIJANA DHIDI YA MATUMIZI YA MIHADARATI


Wito umetolewa kwa viongozi katika jamii hasa wale wa kidini kuchukua jukumu la kuwashauri vijana kama njia moja ya kukabili maovu yanayotokea hasaa visa vya mauaji au uhalifu kila kukicha.
Akizungumza na wanahabari, aliyekuwa naibu gavana kaunti ya Baringo Jacob Chepkwony alirejelea kisa cha mwanamme mmoja eneo la kaptalam, aliyemuua mwanafunzi wa kike wa shule ya upili ya kutwa ya seretunin kwa kumkata kwa upanga akikitaja kuwa cha kusikitisha.
Kulingana na chepkwony iwapo viongozi wa kidini, wa kisiasa, kijamii na pia wazazi watazungumza na kuwashauri vijana basi visa kama hivyo vitaweza kukabiliwa katika siku za usoni.
“Wadau wanapasa kuwafikia vijana na kuwashauri. Iwapo watawaona kama wanasumbuka wanapasa kufahamu kinachowasumbua kwa sababu visa kama hivi havifanyiki tu hivi. Naamini kwamba kuna jambo ambalo lilisababisha kijana huyo kumuua mwenzake. Kwa hivyo ni jukumu la jamii kukishauri kizazi hiki.” Alisema.
Chepkwony alisema kuwa huenda visa vya watu kujihusisha na uovu au mauaji katika jamii vimechangiwa na hali ya vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
“Nafahamu kwamba vijana wetu wanatumia mihadarati. Nawataka kujitenga na tabia hii kwa haya ndio baadhi ya maswala ambayo yanawafanya kutokuwa na tabia ya kupendeza. Ni baadhi ya maswala ambayo yanawapelekea kutekeleza maovu katika jamii.” Alisema.
Wakati uo huo chepkwony aliwahimiza vijana kutafuta ushauri nasaha kutoka kwa viongozi wa kidini au kijamii iwapo wanapitia changamoto mbalimbali katika maisha.