WADAU WATAKIWA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO KATIKA SEKTA YA ELIMU POKOT MAGHARIBI.

Wito umetolewa kwa wadau mbali mbali katika sekta ya elimu kushirikiana na kushughulikia changamoto ambazo zinakabili sekta hiyo kaunti ya Pokot magharibi.

Akizungumza baada ya kuzuru shule mbali mbali kaunti ya Pokot magharibi zinazosimamiwa na kanisa la katoliki, askofu wa kanisa hilo jimbo la Kitale Henry Juma alisema kwamba japo kuna juhudi ambazo zinapigwa, ipo haja ya wadau kushirikiana kuhakikisha kwamba sekta hiyo inaimarishwa.

Askofu juma alitaja uchache wa walimu pamoja na madarasa ya kutosha katika baadhi ya shule kuwa baadhi ya changamoto ambazo zinapasa kushughulikiwa kwa haraka ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata huduma zinazostahili.

“Walimu wamejitolea katika kazi yao lakini licha hayo yote kuna changamoto za hapa na pale ambazo zinapasa kushughulikiwa na wadau wote ikiwemo upungufu wa walimu na madarasa, ili tuwe na mazingira bora ya watoto wetu kuendeleza masomo.” Alisema Juma.

Wakati uo huo askofu Juma alitoa wito kwa bodi za shule kwa ushirikiano na wadau ikiwemo wazazi na viongozi wa dini na wale wa kisiasa kujadiliana na kubuni mikakati itakayohakikisha kwamba nidhamu inadumishwa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanaafikia malengo yao maishani.

“Ningeomba tu kwamba bodi za shule pamoja na wadau wengine kama vile walimu, wazazi viongozi wa makanisa na wale wa kisiasa tuwe macho na tuangalie maswala ya nidhamu miongoni mwa wanafunzi ili tuhakikishe kwamba wanaendeleza masomo na kuafikia ndoto zao maishani.” Alisema.