WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUKABILI UKEKETAJI POKOT MAGHARIBI.

Ukeketaji kwa mtoto wa kike.

Wito umetolewa kwa wadau katika kaunti ya Pokot magharibi kushirikiana na serikali ya gavana Simon Kachapin katika vita dhidi ya utamaduni wa ukeketaji ambao umetajwa kuwa kizingiziti kikubwa kwa elimu ya mtoto wa kike.

Akizungumza wakati akiongoza maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukabili ukeketaji iliyoandaliwa eneo la Nakwiyen, mkewe gavana wa kaunti hiyo Scovia Kachapin alisema kwamba japo takwimu zinaashiria kwamba visa hivi vimepungua, bado kuna kazi ya kufanya kuhakikisha vinamalizwa kabisa.

“Kaunti hii ya Pokot magharibi ilikuwa na visa asilimia 74 vya ukeketaji. Lakini kupitia ushirikiano tumeweza kukabili visa hivi na sasa tuko katika asilimia 44. Hata hivyo asilimia hii inaashiria kwamba tungali na kazi ya kufanya katika kukabili visa hivi.” Alisema Bi. Scovia.

Bi. Scovia alisema kwamba utamaduni wa ukeketaji utaweza tu kukabiliwa iwapo jamii itakumbatia elimu, swala la usawa wa kijinsia na kukabili umasikini, akielezea haja ya kuwapa walioathirika na utamaduni huu huduma za afya, ushauri pamoja na msaada wa kisheria.

“Tutaweza kukabili utamaduni huu wa ukeketaji kupitia kuangazia maswala kama vile elimu, kukabili umasikini pamoja na usawa wa jinsia. Pamoja, tuna nguvu za kukabili utamaduni huu ambao unahujumu hadhi ya mwanamke katika jamii.” Alisema.

Kwa upande wake waziri wa michezo, utamaduni, vijana na huduma za kijamii Lucky Litole aliwataka wazazi katika kaunti hiyo kutowalazimishia wanao utamaduni huu wa ukeketaji na kisha baadaye kuwaoza, na badala yake kuwapa nafasi ya kusoma na kutimiza ndoto zao maishani.

“Ningependa kuwahimiza wazazi kujitenga na utamaduni wa ukeketaji ambao pia hupelekea watoto wasichana waliokeketwa  kuolewa. Waache watoto wasome ili pia waweze kuafikia ndoto zao maishani.” Alisema Litole