WADAU WATAKIWA KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU KACHELIBA.


Mbunge wa kacheliba kaunti ya Pokot magharibi Mark Lumnokol ametoa wito kwa serikali kupitia wizara ya elimu na wadau mbali mbali kuzingatia zaidi eneo hilo katika kuimarisha sekta ya elimu.
Lumnokol amesema kuwa eneo hilo linafaa kuzingatiwa zaidi ili kuwa sawa na maeneo mengine ya nchi kielimu hasa ikizingatiwa sasa wakazi wa eneo hilo wamejitenga na tamaduni zilizopitwa na wakati ikiwemo wizi wa mifugo, ukeketaji na ndoa za mapema na kukumbatia elimu.
Lumnokol amesema eneo hilo la mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda limesalia nyuma kwa muda mrefu kutokana na visa vya ukosefu wa usalama na hali kuwa lilitengwa kwa kipindi kirefu na serikali zilizotangulia.
Wakati uo huo mbunge huyo ametoa wito kwa wanafunzi wote ambao waliathirika kutokana na kufungwa shule kufuatia ujio wa janga la corona, na kupachikwa mimba katika kipindi hicho ila sasa wamejifungua kurejelea masomo ili kuafikia ndoto zao maishani.