WADAU WATAKIWA KUCHANGIA JUHUDI ZA KUHAKIKISHA WATOTO WOTE WANAHUDHURIA MASOMO POKOT MAGHARIBI.

Wadau katika sekta ya elimu kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kushirikiana na idara ya elimu katika kuhakikisha kwamba kila mtoto aliye katika umri wa kwenda shule anahudhuria masomo.

Akizungumza afisini mwake katibu wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la kaunti hiyo ya Pokot magharibi Martine Sembelo aliwataka hasa wazazi kutilia maanani swala la elimu kwa watoto wao kwani itawanufaisha pakubwa katika siku zao za usoni.

Aidha Sembelo aliwataka wazazi na walimu kutowazuia wanafunzi waliopata ujauzito dhidi ya kuendelea na masomo na badala yake kuwapa nafasi hiyo pindi tu wanapojifungua.

“Nawahimiza wadau mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi kwamba twende pale nje na kuangazia zaidi swala hili la watoto kuacha masomo. Ni vyema hata kama mtu amepata mimba arudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua.” Alisema Sembelo.

Sembelo alitaja maeneo ya pokot kaskazini na pokot ya kati kuwa yaliyoathirika zaidi kwa visa vya watoto ambao hawahudhurii masomo japo akipongeza ushirikiano ambao wamepokea kutoka idara ya utawala kuhakikisha kwamba watoto hao wanarejea shuleni.

“Maeneo ambayo yameathirika zaidi na watoto kuacha masomo ni pokot kaskazini na pokot ya kati. Lakini nashukuru kwa sababu watawala wa maeneo haya wanatusaidia kuhakikisha kwamba watoto hawa wanarejea shuleni.” Alisema