WADAU WATAKIWA KUBORESHA MIUNDO MSINGI KATIKA SHULE ZA KAMKETO.


Wadau katika sekta ya elimu kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuisaidia shule ya upili ya wavulana ya Kamketo pamoja na ile ya wasichana hasa upande wa miundo msingi ili kutoa mazingira bora kwa wanafunzi.
Mwalimu mkuu wa shule ya wavulana ya Kamketo Asembo Wesonga amesema shule hiyo inahitaji maabara pamoja bweni la kuwasitiri wanafunzi kwani bweni lililopo kwa sasa halitoshelezi idadi ya wanafunzi katika shule hiyo akitoa wito kwa mbunge wa kacheliba mark lumnokol, serikali ya kaunti pamoja na wahisani kujitokeza na kuhakikisha shule hiyo inashughulikiwa.
Wakati uo huo amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya walimu ambapo kwa sasa ina walimu 4 pekee ambao wameajiriwa na tume ya huduma kwa walimu TSC huku wengine wakiwa wameajiriwa na bodi ya shule hiyo.
Ni wito ambao pia umetolewa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Kamketo ambayo ilianzishwa miaka sita iliyopita Mary Raswei, ambaye ametaka shule hiyo kusaidiwa ili iwe katika nafasi bora ya kutoa mazingira bora ya elimu kwa wanafunzi.
Wakati uo huo Raswei ametoa wito kwa wazazi eneo hilo kutekeleza majukumu yao kama wazazi na kuwaelekeza wanao ipasavyo na kutowaacha kujiamulia hali ambayo huenda ikapelekea kufanya maamuzi yasiyostahili maishani.