WADAU WATAKA MTAALA WA CBC KUAHIRISHWA HADI MIKAKATI THABITI IWEKEWE KUUTEKELEZA.

Jopo la kutathmini utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC likisubiriwa kuandaa ripoti kuhusu vikao lilivyoandaa maeneo mbali mbali ya nchi kutafuta maoni kuhusu mtaala huo, baadhi ya wadau katika sekta ya elimu wanapendekeza utekelezwaji wa mtaala huo kuahirishwa.

Mkurugenzi wa shule ya msingi ya makutano Central katika kaunti hii ya Pokot magharibi Wilbert Mukhwana alisema kwamba hadi kufikia sasa walimu ambao wamepewa mafunzo ya kutekeleza mtaala huo ni wachache mno na itakuwa bora iwapo utekelezwaji wake utaahirishwa kwa muda wa miaka mitatu.

“Tunahitaji walimu zaidi ambao wamefunzwa kuhusu CBC kwa sababu ilivyo sasa waliofunzwa ni wachache mno kwa mtaala huo kutekelezwa. Itakuwa bora iwapo utaahirishwa kwa miaka mitatu ili walimu zaidi wafunzwe kuuhusu.” Alisema Mukhwana.

Wakati uo huo Mukhwana alisema walimu katika shule za upili hawajajiandaa vyema kuwashughulikia wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule za upili daraja ya chini, akipendekeza wanafunzi hao kusalia katika shule za msingi ambako anasema watahudumiwa vyema.

“Walimu ambao wamefunzwa kufikia sasa hata katika shule za upili hawako tayari kuwahudumia watoto hawa. Kwa hivyo watoto hawa watanufaika zaidi iwapo watasalia tu katika shule ambazo wanasomea kuliko kujiunga na shule zingine za upili.” Alisema.