WADAU WATAKA JUHUDI KUELEKEZWA KWA MTOTO WA KIUME KATIKA JAMII


Wadau katika sekta ya elimu kaunti ya Pokot magharibi sasa wanaelezea haja ya juhudi kuelekezwa kwa mtoto mvulana katika jamii kuhakikisha kwamba anapata elimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa madarasa 6 katika shule ya msingi ya Kopoch katika wadi ya Riwo ambayo yalijengwa na wafadhili kutoka taifa la Taiwan, waziri wa elimu kaunti hiyo Rebecca Lotuliatum alisema juhudi zimeelekezwa zaidi kwa mtoto wa kike huku yule wa kiume akitelekezwa.
“Kwa sasa mtoto mvulana ametelekezwa na jamii baada ya juhudi zote kuelekezwa kwa mtoto wa kike. Mtoto wa kike sasa amesoma sana kuliko mtoto wa kiume. Ni wakati ambao wadau wanapasa sasa kuelekeza juhudi kwa mtoto wa kiume ili pia aweze kupata fursa ya kusoma.” Alisema Lotuliatum.
Lotuliatum alitoa wito kwa wazazi kufahamu umuhimu wa elimu kwa wanao wa kiume na kutowatuma kuchunga mifugo na badala yake kuhakikisha kwamba wanahudhuria masomo kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye.
Tunafahamu kwamba jamii ya pokot ni wafugaji na mara nyingi wazazi katika jamii hii huwatuma wanao wa kiume kwenda kulisha mifugo na kutelekeza swala la elimu. Tunawahimiza wazazi kufahamu umuhimu wa elimu kwa wanao na kuwapa fursa ya kusoma na kuimarisha maisha yao ya baadaye.” Alisema.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Samwel Petot ambaye alisema shule hiyo ina wanafunzi wachache zaidi, wengi wao wakisalia nyumbani kutokana na hali kwamba wengi wa wazazi hawafahamu umuhimu wa elimu kwa wanao.
“Wazazi hawaleti wanao shuleni na kuna watoto wengi sana nyumbani wengi wao wakiwa wanatumwa tu kuchunga mifugo. Hivyo nawahimiza wazazi kutia bidii na kuwaleta wanao shuleni ili wapate elimu ambayo itaimarisha hali yao ya maisha.” Alisema Petot.