WADAU WASHINIKIZA KUFUNZWA LUGHA ZA MAMA SHULENI.

Wadau katika sekta ya elimu kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kukumbatia mafunzo ya lugha ya mama shuleni.

Ni wito wake mwanzilishi wa shule ya the Cranes Esther Serem ambaye alisema kwamba wengi wa watoto katika kizazi hiki hawawezi kuzungumza lugha ya mama kutokana na hali kwamba hamna masomo yanayotolewa kwa lugha hizo na badala yake Kiswahili na kiingereza kupewa kipau mbele.

Serem alisema nia yake kuanzisha somo hilo kwenye shule yake ilichochewa na hitaji la mtaala mpya wa elimu CBC ambalo hata hivyo linaegemea zaidi lugha za kigeni kama vile kifaransa, kijerumani miongoni mwa zingine.

“Tuliangalia mtaala mpya wa elimu CBC tukaona kwamba kuna lugha za kigeni ambazo tunafaa kufunza. Lakini sasa tuna lugha zetu pia. Ni kwa nini tusijivunie lugha zetu na tuwafunze watoto lugha za mama? Wengi wa watoto siku hizi wanazungumza tu Kiswahili na kiingereza lakini lugha za mama hawajui.” Alisema Serem.

Aidha Serem ambaye ni mwalimu mustaafu alitoa wito kwa serikali ya kaunti kufadhili uchapishaji wa vitabu ambavyo vimeandikwa kwa lugha ya mama ili kufanikisha juhudi hizo.

“Naishauri serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwamba ikiwezekana watilie mkazo uandishi na uchapishaji wa vitabu vya lugha ya mama ili tusaidie katika juhudi za kuhakikisha kwamba mila zetu hazisahauliki na kukumbatia mila za kigeni.” Alisema Serem.