Wadau wapiga mbio kukomesha dhuluma za jinsia pokot magharibi

Wanchama wa GVRC baada ya kikao cha wadau kuhusu dhuluma za kijinsia, Picha/Benson Aswani
Benson Aswani
Kituo cha Gender Violence Recovery Centre (GVRC) chini ya hospitali ya Nairobi Women kiliandaa kikao jumanne na wadau mbali mbali katika kaunti ya Pokot magharibi kuangazia jinsi ya kukabili visa vya dhuluma za jinsia katika kaunti hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichoandaliwa kwenye mkahawa mmoja mjini Makutano, meneja wa mipango katika kituo hicho Joel Muriithi alisema kando na kuangazia jinsi ya kukabili dhuluma za jinsia kikao hicho pia kililenga kuangazia maswala yanayohusu watu wanaoishi na ulemavu.
“Lengo letu ni kuleta jamii pamoja ili tuwe na mdahalo wa kile kinachofanyika katika kaunti yetu, na jinsi ya kuweka pamoja juhudi zetu kuangazia maswala yanayowakabili kina mama, ikiwemo dhuluma za jinsia,” alisema Muriithi.
Muriithi alisema shirika hilo pia linafanikisha ujenzi wa kituo cha kushughulikia waathiriwa wa dhuluma za jinsia katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria, pamoja na kuwapa mafunzo wahudumu wa afya ambao watakuwa wakiwashughulikia waathiriwa hao.
“Tunajenga kituo cha kushughulikia waathiriwa wa dhuluma za kijinsia katika hospitali ya Kapenguria, wakati uo huo tukiwapa mafunzo wahudumu wa afya kuhusu jinsi ya kuwashughulikia waathiriwa hao,” alisema.
Baadhi ya kina mama ambao walihudhuria kikao hicho wakiongozwa na Eliza Loshiang’ole walitoa wito kwa kina mama kujitokeza na kuripoti visa vya dhuluma za jinsia ili kufanikisha juhudi za kukabiliana na uovu huo katika jamii.
“Sisi kina mama lazima turipoti tukipigwa nyumbani. Kwa hivyo, kina mama tusiogope kuripoti kwa sababu Kenya ya sasa haitaki tena mambo ya dhuluma za kijinsia,” alisema Loshiang’ole.