WADAU WAENDELEZA UHAMASISHO KUHUSU MABADILIKO YA HALI YA ANGA.

Ipo haja kwa serikali za kaunti kubuni na kutekeleza sheria kuhusu mabadiliko ya hali ya anga kando na kubuni bajeti kushughulikia hali hiyo.

Akizungumza baada ya kuongoza kikao na wakazi wa kaunti hii ya Pokot Magharibi kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya anga, afisa katika shirika la CRAWN Trust Cindy Parei  alisema kwamba licha ya kaunti nyingi nchini kuwa na sheria hizo kuhusu mazingira hazizitekelezi.

Parei alisema kwamba vikao vyao hasa vinalenga vijana, kina mama, watu wanaoishi na ulemavu pamoja na wazee lengo kuu likiwa kuwafunza ili kufahamu mabadiliko ya hali ya anga na athari zake kwani ndio huathirika kwa wingi na hali hiyo.

“Mabadiliko ya hali ya anga yanaathiri sote hasa wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu na ni wakati ambapo hatua zinapasa kuchukuliwa. Serikali za kaunti zinafaa kutenga bajeti kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya anga.” Alisema Parei.

Parei aliongeza kwa kusema kwamba, “serikali za kaunti zinapasa kutekeleza sheria zilizopo kuhusu hali ya anga kwa sababu tumetambua kwamba nyingi ya kaunti hizi zina sheria ila hazitekelezi.”

Baadhi ya kina mama ambao walihudhuria mafunzo hayo wakiongozwa na Rosana Kashiol walitaja biashara ya makaa kuwa chanzo kikuu cha mabadiliko ha hali ya anga kutokana na ukataji kiholela wa miti wakipendekeza kuwepo na mbinu mbadala za kujinufaisha.

“Swala la uchomaji makaa si bora. Tunapasa kujaribu kujitenga na uchomaji makaa na tutafute njia nyingine ya kupata mapato na kulisha jamii zetu ila si kwa uchomaji makaa. Na tukiweza pia tuunde makundi ya kupanda miti kwa maboma zetu na hata vijijini.” Alisema Kashiol.