WADAU WA ELIMU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUFANIKISHA SEKTA YA ELIMU KIPKOMO.
Wadau katika sekta ya elimu eneo la Kipkomo kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kushirikiana katika kuhakikisha kuwa viwango vya elimu eneo hilo vinaimarika zaidi.
Akizungumza baada ya kupokea fenicha za afisi kutoka kwa shirikisho la wakuu wa shule za upili KESSHA eneo la Kipkomo, mkurugenzi mpya wa elimu eneo hilo Evans Onyancha, amesema kuwa lengo lake kuu ni kuhakikisha kuwa nidhamu inadumishwa katika sekta ya elimu ili kuhakikisha matokeo bora katika mitihani ya kitaifa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC eneo la Kipkomo Vitalis Oliech ametoa hakikisho la kushughulikiwa uchache wa walimu wa shule za upili eneo hilo ili kufanikisha mpango wa asilimia 100 ya wanafunzi wanaojiunga na shule za upili.
Naye mwenyekiti wa KESSHA eneo hilo Consolata Sortum ameipongeza wizara ya maswala ya ndani ya nchi kwa kutengea eneo hilo afisi maalum akiahidi ushirikiano kutoka kwa walimu kuhakikisha kuwa sekta ya elimu eneo hilo inaimarika zaidi.