Wadau wa elimu waelezea wasiwasi kuhusu hatima ya watoto kielimu pokot ya kati

Na Benson Aswani,
Eneo la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi linakabiliwa na changamoto tele katika sekta ya elimu ambazo zinafanya idadi kubwa ya watoto kukosa elimu.
Akizungumza katika hafla ya kustaafu rasmi, mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC eneo la Pokot ya kati Barnabas Kong’olei alitaja ukeketaji, utovu wa usalama na kutofikiwa baadhi ya maeneo kutokana na miundo mbinu duni kuwa vizingiti kwa baadhi ya watoto kupata elimu.
“Tuna changamoto nyingi katika kaunti hii ambazo zinawafanya wengi wa wanafunzi kukosa kupata elimu kama vile utovu wa usalama, ukeketaji na baadhi ya maeneo kutofikiwa kwa urahisi kufuatia miundo msingi duni,” alisema Kong’olei.
Kauli yake ilisisitizwa na afisa wa mtaala eneo la Sigor Kenneth Chepsiror ambaye aidha alitaja uchimbaji madini kuwa miongoni mwa maswala yanayosababisha idadi kubwa ya watoto kutoenda shule, akiwahimza viongozi kuchukua jukumu la kuwahamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa wanao.
“Uchimbaji madini pia umeathiri masomo eneo hili, wengi wa watoto hasa wavulana wakijitosa kwenye shughuli hiyo. Nawasihi viongozi eneo hili kuwahamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa wanao,” alisema Chepsiror.
Kwa upande wa mkurugenzi wa elimu kaunti ndogo ya Kipkomo Evans Onyancha alipongeza juhudi ambazo zinaendelezwa na viongozi kuhakikisha kwamba elimu inaimarika katika kaunti hiyo kupitia basari ambazo wamekuwa wakitoa kwa wanafunzi.
“Elimu imeimarika katika kaunti hii kutokana na juhudi za viongozi kuona kwamba watoto wanapata elimu, kupitia kutoa basari kwa wanafunzi ambazo zimesaidia pakubwa kuhakikisha kwamba wanasalia shuleni,” alisema Onyancha.