Wadau wa elimu Pokot magharibi wapongeza kuzinduliwa basari na serikali ya kaunti

Na Emmanuel Oyasi,
Wadau mbali mbali katika sekta ya elimu kaunti ya Pokot magharibi wamepongeza hatua ya kuzinduliwa basari ya serikali ya kaunti katika hafla ambayo iliandaliwa ijumaa iliyopita katika shule ya upili ya Chesta eneo bunge la Sigor.


Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Chesta Patricia Nandi alisema fedha hizo ni muhimu katika kuhakikisha elimu kwa wanafunzi ikizingatiwa wengi wao wanatoka katika jamii ambazo hazijiwezi kifedha, wakitegemea fedha za basari kwa asilimia kubwa ya karo.


“Wakati hakuna basari wanafunzi wengi hawaji shuleni. Katika hali ya kuwa nyumbani wanajikuta ni wajawazito na hatimaye kuacha masomo,” alisema Bi. Nandi.


Aidha Nandi alisema shughuli nyingi za shule hutegemea pesa kutoka kwa serikali hasa basari, na kuchelewa kutolewa fedha hizo kulikuwa kumelemaza pakubwa shughuli katika shule na hivyo kuathiri viwango vya elimu ambavyo vinatolewa.


“Wakati pia hatuna pesa shuleni shughuli haziendeshwi vizuri hali ambayo inaathiri hata matokeo ya wanafunzi wetu. Lakini wakati umepewa pesa kama hizi unaweza kupanga na ufanye mambo mazuri,” alisema.


Kando na hayo Nandi alilalamikia kukithiri mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi hasa eneo la pokot kaskazini, akitoa wito kwa wazazi kuwa karibu na wanao na kuwashauri kila mara, na pia kufuatilia kwa karibu mienendo yao ili waweze kukamilisha masomo yao vyema.


“Visa hivi havijapungua. Bado tunavishuhudia katika shule za maeneo haya. Wanafunzi wengi wakifika kidato cha pili hutoka shuleni kwa sababu ya mimba za mapema. Kwa hivyo, wazazi wanapasa kuwaweka watoto wao karibu na kufuatilia mienendo yao,” aliongeza.