WADAU POKOT MAGHARIBI WAONYWA DHIDI YA KUFANIKISHA WIZI WA MITIHANI YA KITAIFA.

Mitihani ya kitaifa kwa ajili ya darasa la nane KCPE na kidato cha nne KCSE ikiendelea kukaribia, wadau katika sekta ya elimu kaunti hii ya Pokot magharibi wameonywa dhidi ya jaribio lolote la kufanikisha udanganyifu katika mitihani hiyo.

Katikabu mkuu wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la Pokot magharibi Enrico Martine Sembelo amesema kwamba wanafunzi wanafaa kupewa fursa ya kufanya mitihani hiyo wenyewe na kupata kile wanachostahili kulingana na uwezo wao.

Sembelo hata hivyo ameelezea imani yake kwamba watahiniwa watafanya vyema katika mitihani hiyo kulingana na maandalizi ambayo wamepokezwa na walimu wao.

“Tuache watoto wafanye mitihani yao na wapate kile watakachopata. Tunataka matokeo ambayo hayatakuwa na dukuduku mwaka huu na nina imani kwamba watoto wetu watafanya vyema katika mitihani hiyo. Wadau wote katika mitihani hii wanafaa kujitenga na jaribio lolote la kufanikisha wizi wa mitihani.” Alisema Sembelo.

Wakati uo huo Sembelo ametoa wito kwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin kuharakisha na kutimiza ahadi yake ya kutoa fedha za basari kwa ajili ya wanafunzi akisema kuwa wazazi wengi wanasubiri ufadhili huo kwa wanao.

“Naishukuru serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi chini ya gavana Simon Kachapin kwa kuahidi kutoa basari kwa wanafunzi kutoka jamii zisizojiweza. Tunachoomba ni kwamba aharakishe kutimiza ahadi hiyo kwani jamii nyingi sasa zinasubiri fedha hizo.” Alisema.