WADAU MBALI MBALI WAENDELEA KUPINGA UAMUZI WA MAHAKAMA KUHUSU HARAKATI ZA LGBTQ NCHINI.
Viongozi mbali mbali wa kidini wameendelea kukosoa uamuzi wa mahakama ya upeo wa kuwaruhusu watu wanaoendeleza mahusiano ya jinsia moja kubuni mashirika ya kutetea maslahi yao.
Wa hivi punde kuzungumzia swala hili ni mchungaji wa kanisa la AIC Cheptia katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Musyoka ambaye alisema kwamba hatua hiyo ni kinyume cha maadili ya kikristo na tamaduni za kiafrika.
Alitoa wito kwa majaji kutafakari kuhusu athari za maamuzi yao kabla ya kuafikia uamuzi wowote ambao huenda ukapelekea kupotoka zaidi maadili ya jamii.
“Tunashangaa sana kuona kwamba mahakama inahalalisha makundi yanayoendeleza mapenzi ya jinsia moja na hata kutambua mashirika yao. Hii ni kinyume kabisa na tamaduni za kiafrika na maandiko ya biblia. Mahakama pia zinafaa kutafakari kuhusu athari za maamuzi ambayo zinatoa nchini.” Alisema Musyoka.
Aidha Musyoka alimpongeza rais William Ruto kwa kutangaza msimamo wa kupinga mahusiano hayo akitoa wito pia kwa viongozi wa kidini kusimama kidete na kupinga kuendelezwa mahusiano hayo humu nchini.
“Nampongeza sana rais Ruto kwa kuchukua msimamo kuhusiana na mahusiano haya nchini. Nawaomba viongozi wote wa kidini kusimama kidete na kupinga tabia hii kabla ya ghadhabu ya Mungu kutushukia.” Alisema.