Wabunge waelezea hofu ya usalama kufuatia mauaji ya Were

Peter Lochakapong mbunge wa Sigor kaunti ya pokot magharibi, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Viongozi wa matabaka mbali mbali nchini wameendelea kutoa hisia zao kuhusiana na mauaji ya mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were.
Wakiongozwa na mbunge wa Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong, viongozi hao wamewasuta maafisa wa usalama kwa kile wamedai kuzembea kazini hali ambayo ilipelekea mbunge huyo kuuliwa wakati mauaji yake yangezuiwa.
Lochakapong alilalamikia hali kwamba marehemu Were alikuwa amerekodi taarifa katika kituo cha polisi kwamba maisha yake yamo hatarini baada ya kushuku kufuatwa na watu fulani, ila taarifa yake haikushughulikiwa na maafisa wa usalama.
“Wale ambao wanahusika katika kuhakikisha usalama wa wakenya hasa viongozi wanapasa kuwajibika kwa sababu haiwezekani kwamba mbunge huyo alikuwa ameandikisha taarifa kwamba maisha yake yamo hatarini na hamna hatua ambayo ilichukuliwa,” alisema Lochakapong.
Lochakapong sasa anawataka maafisa wa usalama kuwajibika na kuhakikisha usalama wa viongozi waliochaguliwa na wananchi kwa ujumla akisisitiza kuwa kitendo cha kuuliwa mbunge Were sasa kinawatia hofu viongozi wengine nchini.
“Kile ambacho nitasema ni kwamba serikali iweze kuimarisha usalama wa viongozi hasa wale ambao wamechaguliwa, kwa sababu kitendo kama hiki kitawatia hofu viongozi nchini,” alisema.