WAATHIRIWA WA MAFURIKO MUINO WALALAMIKIA KUTELEKEZWA NA SERIKALI
Waathiriwa wa mafuriko ya mwaka 2019 eneo la Muino Pokot ya kati kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kutelekezwa na serikali licha ya hasara na madhara waliyopata kufuatia hali hiyo.
Wakiongozwa na David Chilo, waathiriwa hao walisema kwamba licha ya kuwasilisha malalamishi yao kwa serikali ya kaunti walipohitajika kufanya hivyo, hamna hatua yoyote ambayo imechukuliwa hadi kufikia sasa huku wakidai kuendelea kupitia hali ngumu kufuatia madhara yaliyowakuta.
Walisema kwamba wanalizimika kutegemea vibarua ili angalau kukimu mahitaji ya familia zao, hali wanayosema hata hivyo haiwatoshelezi kufuatia kupanda gharama ya maisha.
“Tuliathirika sana kwa mafuriko ambayo yalishuhudiwa eneo hili mwaka 2019. Serikali ya kaunti ilitaka majina ya watu ambao waliathirika na mafuriko hayo lakini licha ya kuwasilisha majina yetu, hakuna msaada ambao tulipokea hadi sasa. Kwa sasa tunapitia hali ngumu ya maisha kufuatia hali hiyo.” Walisema.
Walitoa wito kwa serikali ya kaunti kuwasaidia kukidhi mahitaji yao na familia zao kwani sasa wanakabiliwa na tatizo la chakula pamoja na karo kwa ajili ya wanao ikizingatiwa hawajapiga hatua yoyote kimaisha tangu wakati huo.
“ Tunaomba serikali ya kaunti iwapo kuna njia yoyote ambayo inaweza kutusaidia tafadhali ifanye hivyo kwa sababu tumehangaika sana. Tuna njaa na watoto wetu wameshindwa kwenda shule kwa ukosefu wa karo.” Walisema.
Hata hivyo mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alikana kuwepo waathiriwa ambao walikosa kusaidiwa na serikali akisema kwamba wengi wa waathiriwa hao walipokea msaada ambao ulikusudiwa kuwawezesha kuanzisha upya maisha yao.
“Ninachofahamu ni kwamba wote ambao waliathirika hapa na mafuriko walipata msaada. Hata wengi walijengewa nyumba. Tulikuja hapa siku hiyo na kuwapa watu chakula. Kwa hivyo kiwango ambacho serikali imefanya kuwasaidia ni kikubwa. Hivyo sioni kama kuna mtu ambaye aliachwa.” Alisema Lochakapong.