VYAMA VYA SIASA VYATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA UCHAGUZI.


Tume ya uchaguzi nchini IEBC imetoa wito kwa vyama vya kisiasa kaunti hii ya Pokot magharibi kuhakikisha kwamba vinazingatia sheria za uchaguzi kikamilifu taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi agosti.
Akizungumza baada ya kikao na maajenti wa vyama mbali mbali vya kisiasa kaunti hii pamoja na afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa, msimamizi wa uchaguzi katika tume hiyo kaunti hii Joyce Wamalwa amevitaka vyama hivyo kuwadhibiti wafuasi wao ili kuhakikisha kuwa amani inadumu katika kaunti hii.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na afisa katika afisi ya msjili wa vyama vya kisiasa Lorta Erukudi ambaye aidha amevitaka vyama vya kisiasa kutilia maanani yaliyoafikiwa katika kikao hicho wakati vikiwatuma maajenti wake kwenye vituo mbali mbali vya kupigia kura.
Ajenti mkuu wa chama cha UDA katika kaunti hii ya Pokot magharibi Benson Rajab amevitaka vyama vya kisiasa kuwekeza zaidi kwenye maajenti wake huku pia akiitaka wizara ya usalama wa ndani ya nchi kuhakikisha kuwa amani inadumu kipindi hiki cha uchaguzi.