VITA VYA UKRAINE HAVIJAATHIRI GHARAMA YA MAISHA NCHINI; ASEMA RUTO


Mgombea urais wa chama cha UDA William Ruto amepuuzilia mbali madai ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba gharama ya juu ya maisha kwa sasa imechangiwa pakubwa na vita baina ya Ukraine na Urusi.
Ruto amesema suluhisho la kupunguza gharama ya maisha ni kuwekeza katika kilimo na kuongeza uzalishaji wa wakulima maradufu.
Mnamo Mei 1, 2022 wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi katika bustani ya Uhuru, rais Kenyatta aliwataka wanasiasa akiwemo Ruto kukoma kumlaumu kwa gharama ya juu ya maisha nchini.
Alimkemea naibu wake akisema mzozo wa sasa uko nje ya uwezo wake kwani ulisababishwa na sababu kama vile janga la Covid-19 na mzozo wa Urusi na Ukraine.
Hata hivyo, alipokuwa akizungumza Ijumaa usiku wakati wa uzinduzi wa manifesto ya Kenya Kwanza katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, Ruto alisema gharama ya sasa ya maisha imesababishwa na gharama kubwa ya pembejeo za kilimo.
Hata hivyo licha ya kusema kwamba vita hivyo havijaathiri gharama ya maisha humu nchini, kiongozi huyo alidokeza kwamba athari zake ni mojawapo ya changamoto tatu ambazo zimelemaza uchumi wa taifa.