VISA VYA NDOA ZA MAPEMA BADO VINASHUHUDIWA ENEOBUNGE LA KACHELIBA

Wadau mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia kuendelea kushuhudiwa visa vya ndoa pamoja na mimba za mapema kwa watoto wa kike licha ya juhudi ambazo zinawekwa katika kuhakikisha kwamba visa hivi vinakabiliwa.

OCS wa kacheliba Tom nyangau amesema kwamba polisi eneo hilo waliwaokoa watoto wa kike wanne ambao walikuwa wameozwa na wazazi wao katika kipindi cha juma moja ambacho shule zilifungwa, wawili wakiwa wanafunzi wa shule za msingi na wawili ambao walikuwa tayari wameacha masomo.

Nyangau  amesema kwamba wengi wa wazazi eneo hilo wanawaoza mapema wanao lengo kuu likiwa kupata mali kutokana na mahari inayolipwa na wanaowaowa watoto hao.

Wakati uo huo nyangau amesema vingi vya visa hivi huchangiwa na baadhi ya tamaduni katika kaunti hii ambapo watoto wa kike wanaruhusiwa kutangamana kiholela na wenzao wa kiume akionya kuwa watakaopatikana wakishiriki tamaduni hizo watakabiliwa kisheria.

Hata hivo nyangau amesema kuwa wanaendeleza uhamasisho kwa wakazi dhidi ya visa vya ndoa za mapema na athari zinazotokana na visa hivyo pamoja na kuwahimiza kuhakikisha kwamba wanawapelekea wanao shuleni kwa manufaa yao ya baadaye.