VISA VYA MIMBA ZA MAPEMA VYAKITHIRI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI
Visa vya mimba za mapema miongoni mwa wasichana katika kaunti ya Pokot Magharibi vinazidi kuongezeka kila kuchao huku mashirika mbalimbali yakiingilia kati suala hilo zima katika kuwahimiza wazazi kukaa karibu na watoto wao wa kike ili kuinusuru hali hiyo.
Kulingana na Winnie Cheptoo afisa katika shirika la kuangazia masuala ya mtoto wa kike katika kaunti za maeneo kame SIKOM, amesema kaunti hii imerekodi visa hivyo zaidi ya mia nane kila mwezi tangu janga la korona lilipolipuka humu nchini.
Cheptoo amewataka wazazi kuwalinda wanao na kuwashauri dhidi ya maadili potovu katika jamii hasa muda huu ambapo sherehe nyingi zinatarajiwa kuandaliwa mwezi wa Disemba.
Aidha ameendelea kuwahimiza wazazi kukoma kushikilia tamaduni zilizopitwa na wakati zikiwamo ukeketaji, kuoza mabinti mapema miongoni mwa nyingine huku akitaja hali hiyo kuwa dhuluma kuu miongoni mwa wasichana wa jamii ya Pokot.