VISA VYA KUDUMAA NA UTAPIA MLO VYAPUNGUA POKOT MAGHARIBI.
Visa vya kudumaa katika ukuaji miongoni mwa watoto katika kaunti hii ya Pokot magharibi vimepungua kutoka asilimia 45 mwaka 2014 hadi asilimia 35 kufikia mwaka 2019 kulingana na takwimu za shirika la action agaist hunger.
Akizungumza wakati wa kukabidhi wizara ya afya kaunti hii ya pokot magharibi vifaa vya kukabili utapia mlo pamoja na kudumaa katika ukuaji miongoni mwa watoto, meneja wa mipango katika shirika hilo kaunti hii Salome Tsindori amesema kuwa hilo limeafikiwa kufuatia mikakati ambayo imewekwa na serikali ya kaunti.
Aidha Tsindori amesema visa vingi vya utapia mlo vinatokana na hali kuwa kina mama katika kaunti hii ndio walio na majukumu mengi katika jamii hivyo kutokuwa na wakati wa kutosha kumnyonyesha mtoto inavyopasa.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na waziri wa afya kaunti hii Christine Apakoreng ambaye pia amesema kuwa kuna maafisa wa afya ambao wametumwa nyanjani kutoa elimu kwa kina mama kuhusu jinsi ya kuwalisha wanao ili kukabili swala la utapia mlo.