VISA VYA HIV MIONGONI MWA WATOTO POKOT MAGHARIBI VYATAJWA KUONGEZEKA.

Ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuhakikisha kuwa anamlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba za mapema na maambukizi ya virusi vya HIV.

Ni wito wake afisa katika shirika linaloshughulikia idadi ya watu na maendeleo national council for Population and development NCPD Janet Lunai ambaye alisema kwamba ngono za mapema miongoni mwa watoto zimechangia ongezeko la watoto wanaougua virusi vya HIV.

Akizungumza katika hoteli ya Horizon viungani mwa mji wa makutano kaunti hii ya Pokot magharibi wakati wa kikao cha wadau kuangazia hali ya HIV kaunti hii, Lunai alisema kwamba kwa sasa ni asilimia 42 ya watoto kati ya miaka 10 hadi 24 wanaougua HIV hali ambayo ni ya kutia wasi wasi.

“Kama kuna mimba katika umri mdogo ina maana kwamba hawakutumia kinga wakati wa ngono. Na hii ndiyo sababu kuna maambukizi mengi ya HIV miongoni mwa watoto wenye kati ya umri wa miaka 10 hadi 24 ambapo ni asilimia 42. Hali hii inatutia wasi wasi sana na hivyo inafaa kuwa jukumu la kila mmoja kuwachunga watoto wenye umri huo.” Alisema Lunai.

Kwa upande wake msimamizi wa maswala ya HIV katika kaunti hiyo Clement Kibet alisema kwamba idadi ya maambukizi Pokot magharibi imechangiwa na kutoripotiwa visa vya dhuluma za kijinsia ambapo baadhi ya watoto wa kike wanadhulumiwa kingono na maswala hayo kusuluhishwa nyumbani bila hata mtoto kupimwa iwapo ameambukizwa.

“Tukiangalia takwimu ni asilimia 20 pekee ya visa vya dhuluma za kijinsia ambavyo huripotiwa hospitalini na kisha kuelekezwa kwa polisi. Na wale ambao mara nyingi hufika ni wale ambao wamepata mimba ila asiposhika mimba visa hivyo haviripotiwa. Hali hii imechangia wengi wa watoto kupatikana na virusi vya HIV.” Alisema Kibet.