VISA VYA DHULUMA DHIDI YA WAKENYA SAUDI ARABIA VYAENDELEA KURIPOTIWA.

Familia ya Betty Wanjala mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na mkaazi wa kijiji cha Pombo mtaani lesos katika kaunti ya Trans nzoia imeomba serkali kuingilia kati na kumrejesha binti wao ambaye anaaminika kuugua kutokana na mateso mikononi mwa mwajiri wake katika taifa la saudi Arabia.

Mamaye Finike Onduso amewaambia wanahabari kwamba mawasiliano yamekatizwa baada ya mwajiri wake kumpokonya simu yake.

“Wakati alifanya kazi miezi tisa ikakamilika, mwajiri wake akamwambia hamna pesa. Alipouliza ni kwa nini akaanza sasa kuteswa na kutishiwa maisha. Amepokonywa paspoti yake na hata simu na sasa kuwasiliana naye imekuwa vigumu. Alipo ni mgonjwa sana ila hana msaada.” Alisema.

Dadaye Emmah wanjala anasema kwamba hali ya afya yake inaendelea kudhoofika mno na kwamba hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa ili kumnusuru.

“Mateso anayopokea yamempelekea kupata ugonjwa wa moyo, na hata figo zina matatizo na tunaambiwa tunaweza kumpoteza wakati wowote. Tunaomba kwamba mtoto wetu arejee salama.” Alisema.

Mwakilishi wa wadi ya bidii James Mwangi ambaye amefika katika boma la msichana huyo ameirai serikali kuweka sheria kali za kuwawajibisha maajenti wanaowatelekeza kwa wateja wao.

 “Kunapasa kuwepo na sheria ambazo zitawawajisha maajenti ambao wanafanikisha kuelekea wakenya katika taifa la Saudi Arabia iwapo jambo lolote litatokea kwa wakenya hao.” Alisema Mwangi.

Visa vya wasichana kudhulumiwa nchini saud Arabia vinaendelea kuripotiwa huku serikali ikiombwa kuweka mikakati ya kukabili hali hiyo.