Viongozi watakiwa kusitisha siasa na kuangazia maendeleo kwa wananchi

Simon Kachapin Gavana Wa Kaunti Ya Pokot Magharibi, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Wito umetolewa kwa viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi kusitisha siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 na badala yake kutumia wakati huu kushughulikia ahadi walizotoa kwa wananchi wakati wa msimu wa kampeni.


Ni wito ambao umetolewa na gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin ambaye amelalamikia hali ya siasa ya sasa, akisema hali hii inapelekea kulemazwa maendeleo yanayokusudiwa kuwanufaisha wananchi.


“Kuna wakati wa kila kitu, siasa za mapema si nzuri. Nchi haiwezi kuendelea kwa kuendeleza siasa za kila wakati. Uchaguzi ulikamilika na ni wakati viongozi wanapasa kuangazia yale waliwaahidi wananchi,” alisema Kachapin.


Aidha Kachapin alishutumu makundi ya kisiasa ambayo yamechipuka katika kaunti hiyo aliyosema yanatumika kuwachafulia wapinzani majina, hali aliyosema huenda ikachochea migawanyiko miongoni mwa wakazi.


“Sasa kuna makundi ya kisiasa ambayo yameibuka katika kaunti hii na yanatumika kueneza chuki, matusi na kuwaharibia wanasiasa wengine majina,” alisema.


Akiwataka viongozi kukoma kuendeleza siasa za ubinafsi na kujitakia makuu, na badala yake kuangazia changamoto ambazo zinawakumba wananchi na kusubiri hadi uchaguzi mkuu ujao kabla ya kushiriki siasa.


“Tusiweke sana maslahi yetu mbele kuliko wale waliotuchagua. Ni wakati kama viongozi tunapasa kuangazia changamoto ambazo zinawakumba wananchi. Wakati wa uchaguzi utafika na tutapiga siasa wakati huo,” aliongeza.