VIONGOZI WATAKIWA KUHAKIKISHA KWAMBA USALAMA UNAIMARISHWA WAKATI HUU WA KAMPEINI NA BAADA YA KAMPEINI
Idara ya polisi katika kaunti hii ya Pokot magharibi imetoa wito kwa wanasiasa kuhakikisha kuwa amani inadumishwa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwezi agosti ili kila mmoja apate nafasi ya kuendeleza kampeni zake bila kusumbuliwa.
Akizungumza baada ya kikao na wagombea nyadhifa mbali mbali kamanda wa polisi kaunti hii Peter Katam amewataka wagombea nyadhifa za kisiasa kuhakikisha kuwa wafuasi wao wanadumisha nidhamu kabla wakati na hata baada ya uchaguzi wa mwezi agosti.
Aidha Katam amewataka wagombea wote wa kisiasa kuhakikisha kuwa wanakamilisha kampeni zao saa kumi na mbili jioni, pamoja na kutoendesha kampeni zao maeneo rasmi kama vile hospitali ili kuzuia kelele maeneo hayo.
Aidha ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao kueneza propaganda pamoja na semi za chuki akionya kwamba idara ya usalama itafuatilia matumizi ya mitandao na atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali za sheria.