VIONGOZI WATAKA MTAALA WA CBC KUANGAZIWA KWANZA POKOT MAGHARIBI


Itakuwa vigumu kwa mtaala mpya wa elimu CBC kutekelezwa kwa ufanisi katika kaunti hii ya Pokot magharibi iwapo changamoto zinazoambatana na utekelezwaji wa mtaala huo hazitashughulikiwa kabla ya kutekelezwa.
Akizungumza na kituo hiki seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio amesema kuwa wizara ya elimu haikutilia maanani hali katika kaunti hii ya Pokot magharibi kabla ya kuanza kutekeleza mtaala huo akisema kuwa kaunti hii imetengwa pakubwa katika utekelezwaji wake.
Poghisio ametoa wito kwa idara ya elimu ikiongozwa na waziri wa elimu prof. George Magoha kuhakikisha kuwa kaunti hii inashughulikiwa ikiwemo maswala ya miundo msingi na kuisawazisha na kaunti zingine kabla ya kutekelezwa mtaala huo.
Wakati uo huo seneta Poghisio ameelezea haja ya serikali ya kaunti hii kuwekeza pakubwa katika elimu ya watu wazima ili kutoa fursa kwa wazazi ambao hawakupata fursa ya kwenda shule kuhudhuria masomo ili kuwaweka katika fursa nzuri ya kuwasaidia wanao kulingana na hitaji la CBC.