VIONGOZI WATAKA KUWEKWA MIKAKATI YA KUKABILI HALI YA UKAME KATIKA KAUNTI ZA WAFUGAJI

Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi sasa wanatoa changamoto kwa serikali ya rais William Ruto kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba swala la ukame linakabiliwa hasa katika kaunti za wafugaji kulingana na ahadi yake.

Wakizungumza eneo la Riwo, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto walisema swala la ukame limekuwa changamoto kuu kwa wakazi wa kaunti hizi ambapo wengi wao wamekadiria hasara kubwa kila msimu wa kiangazi kwa kupoteza mifugo yao.

“ Hali ya kiangazi imekuwa mbaya zaidi maeneo haya hadi wakulima wengi wamekadiria hasara kufuatia kufa mifugo yao. Kwa hivyo ni wakati ambapo serikali inapasa kuona jinsi ambavyo maji yatapatikana maeneo haya ili kuokoa wananchi na mifugo yao.” Alisema Moroto.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na viongozi eneo hilo la Riwo wakiongozwa na mwakilishi wadi wa eneo hilo David Alukulem ambao aidha waliitaka serikali kutimiza ahadi yake ya kuleta chakula cha msaada kwa wakazi ambao wanapitia hali ngumu.

“Wanyama wengi maeneo haya wamedhoofika na hali si hali. Wakazi hawana chakula na wanategemea sana matunda ya mwituni. Serikali inapasa kutimiza ahadi yake kwamba ingeleta chakula kwa ajili ya wakazi kwa sababu sasa wanahangaika.” Walisema.

Wakazi wa eneo hilo walielezea kupitia wakati mgumu kupata maji wakitoa wito kwa serikali kuingilia kati ili kuwachimbia visima.

“Tuna changamoto kubwa ya kupata maji safi ya matumizi nyumbani. Tunalazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Tunaomba viongozi wetu kutuchimbia visima ili tupate maji.” Walisema wakazi.