VIONGOZI WATAJA MBINU MBOVU ZINAZOTUMIKA KUKABILI UTOVU WA USALAMA KASKAZINI MWA BONDE LA UFA KUWA CHANZO CHA KUKITHIRI TATIZO HILO.
Serikali inapasa kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inaanzishwa katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa ambazo zinakabiliwa na utovu wa usalama unaosababishwa pakubwa na wezi wa mifugo.
Haya ni kwa mujibu wa viongozi kutoka kaunti hizi wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto, ambao walisema kwamba visa vya uvamizi vitakabiliwa kabisa iwapo kutakuwa na maendeleo maeneo hayo, badala ya oparesheni za kila mara ambazo hazileti matunda.
Viongozi hao walisema kwamba mbinu hiyo ilitumika awali maeneo yaliyokuwa sugu katika visa vya utovu wa usalama ikiwemo mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Trans nzoia, na kuleta ufanisi mkubwa.
“Tulikuwa na shida kati ya Pokot magharibi na Trans nzoia miaka ya hapo nyuma. Lakini wakati jeshi lilikuja likaleta maji na maendeleo mengine, hiyo shida iliisha. Sasa hata hili tatizo lilopo kwa kaunti hizi sita linahitaji tu maendeleo na litaisha. Si jambo lingine, ni maendeleo tu.” Alisema Moroto.
Wakati uo huo viongozi hao walimtaka waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuandaa kikao na viongozi wa kaunti hizi, ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo hili, na kuwezesha kuafikiwa maendeleo kwenye maeneo haya.
“Kindiki anafanya kazi peke yake. Hahusishi viongozi wa maeneo haya. Kile tunachoomba ni Kindiki ashirikiane na viongozi wa kaunti hizi ambao wanafahamu hali ilivyo ili kutafuta suluhu ya kudumu.” Walisema.