VIONGOZI WASHUTUMU MASHAMBULIZI AMBAYO YAMEENDELEA KURIPOTIWA LICHA YA OPARESHENI INAYOENDELEA BONDE LA KERIO.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu vikali mashambulizi ambayo yameendelea kuripotiwa katika kaunti za bonde la kerio licha ya oparesheni ya kiusalama ambayo inaendelea katika kaunti sita za kaskazini mwa bonde la ufa.

Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto viongozi hao aidha walilaumu matamshi ambayo yanatolewa na baadhi ya wanasiasa kutaka jamii fulani kuhama maeneo yao wakiashiria kwamba huenda ndio wanatekeleza visa vya uvamizi wakisema matamshi kama hayo ndiyo yanayozidisha uhasama maeneo haya.

“Nawalaumu wanasiasa hasa wale ambao ni chipukizi. Wanafikiri kwamba kupiga domo ndio kuleta maendeleo au ndio wataonekana kuwa ndio sasa kupendeza wananchi. Wengi wao wamekuwa wakiropokwa maneno ambayo yamechochea pakubwa uhasama miongoni mwa jamii za eneo hili.” Alisema Moroto.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi ya Riwo David Alukulem ambaye alitaka serikali kuwachunguza viongozi ambao wanaeneza uchochezi miongoni mwa wakazi wa kaunti hizi na kuwachukulia hatua ili kuhakikisha jamii zote za eneo hili zinaishi kwa amani.

“Serikali ina macho ya kuona mahali ambako uchochezi unatokea. Kuna wale ambao wanaonekana wazi wakieneza uchochezi na nafikiri kufikia sasa serikali imewaona. Sisi kama viongozi wa sehemu hii tunasema serikali ifanye kazi yake na kuwakabili viongozi wanaochochea raia.” Alisema Alukulem.

Kwa upande wake aliyekuwa mwaniaji kiti cha mwakilishi wadi ya Riwo Joel Limakina alielezea haja ya wazee katika kaunti hizi kutumika katika kutafuta amani kwa kuandaa vikao na pande zote akitaja swala la malisho na maji kuwa chanzo kikuu cha utovu wa usalama maeneo haya.

“Hamna shida yoyote ambayo itaweza kutatuliwa bila kuwahusisha wazee. Wazee wanapasa kupewa kipau mbele katika kuandaa mazungumzo ya kuhakikisha kwamba jamii za pande zote zinazohusika zinasitisha uhasama ambao huenda unasababisha utovu huu wa usalama.” Alisema Limakina.

[wp_radio_player]