VIONGOZI WAONYWA DHIDI YA KUWATUMIA VIJANA KUZUA VURUGU.


Siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka ujao zikiendelea kushika kasi, wito umetolewa kwa viongozi wa siasa nchini kutowatumia vijana kuwashambulia wapinzani wao na kuzua vurugu katika mikutano mbali mbali ya kisiasa.
Ni wito wake katibu katika wizara ya michezo, utamaduni na toradhi za kitaifa Simon Kachapin ambaye amewataka viongozi kuendesha kampeni zao kwa njia ya amani ili kuwapa nafasi wananchi kufanya uamuzi wao katika mazingira salama kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Aidha kachapin ambaye alikuwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi amewataka vijana kutokubali kutumika na wanasiasa kwa kupewa fedha ili kuzua vurugu, na badala yake kutumia muda wao kuwapiga msasa ili kuhakikisha wanawachagua viongozi ambao watawahudumia inavyostahili.
Wakati uo huo Kachapin ametoa wito kwa vijana ambao wametimu umri wa kupiga kura kuhakikisha kuwa wanajisajili katika zoezi la kuwasajili wapiga kura linaloendelea nchini ili kuwa katika nafasi ya kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia wa kuwachagua viongozi bora.