VIONGOZI WALALAMIKIA UTOVU WA USALAMA KERIO VALLEY.


Viongozi katika kaunti ya Elgeyo marakwet sasa wanaitaka serikali kuu kupitia idara ya usalama kuwapa uhamisho maafisa wa usalama wanaohudumu kwenye eneo la bonde la kerio.
Wakiongozwa na mbunge wa Marakwet mashariki Kangogo Bowen viongozi hao wamesema kuwa maafisa hao wamefeli kutekeleza jukumu lao la kuwahakikishia wenyeji ulinzi.
Akirejelea uvamizi uliotekelezwa kwenye eneo bunge hilo siku ya jumamosi na ambapo watu wanne waliuwawa na idadi ya mifugo isiyojulikana kuibwa Bowen aidha ameitaka serikali kuwaajiri maafisa wa polisi wa akiba ili kusaidia katika kuwakabili wahalifu.
Kwa upande wake naibu gavana kaunti hiyo Wesley Rotich amemtaka rais Uhuru Kenyatta kuzungumzia hali ya utovu wa usalama katika bonde le kerio na vile vile kuagiza kuanzishwa oparesheni ya kutwaa silaha mikononi mwa wahalifu anaosema wanatoka kwenye kaunti jirani.