VIONGOZI WAKASHIFU MAUAJI YA CHESOGON.


Viongozi kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu mauaji ya watu watatu wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi yaliyotekelezwa na washukiwa wa uhalifu eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.
Wa hivi punde kulaani mauaji hayo ni seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye ametaka idara za usalama kuwatafuta wahalifu waliohusika katika mauaji hayo na kuhakikisha kuwa wanachukuliwa hatua za kisheria na kuwapokonywa bunduki wanazotumia kutekeleza uhalifu.
Aidha Poghisio ameendelea kusisitiza umuhimu wa viongozi kutoka pande zote mbili kuandaa mazungumzo na wakazi wa kaunti hizi ili kuhakikisha kuwa amani inaafikiwa maeneo haya ya mpakani ambayo yameshuhudia utovu wa usalama kwa muda sasa.
Wakati uo huo Poghisio ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuendelea na shughuli za kawaida japo kwa kuzingatia umakini zaidi hasa kwa wanafunzi wanaoelekea shuleni pamoja na walimu.