VIONGOZI WAENDELEA KULAUMU UONGOZI WA GAVANA WA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI


Mwakilishi Maalum Ozil Kasheusheu ameendelea kumlaumu Gavana Lonyangapuo kwa madai ya kukawia kwa miradi mingi iliyokuwa kwenye manifesto yake.
Akizungumza katika Kipindi Cha Mpigo wa Kalya Radio leo asubuhi, Ozil ametaja uongozi wa Lonyangapuo kuwa wenye ubaguzi mkubwa akisema wawakilishi wa Wadi ambao wamekuwa wakiupinga uongozi wake wamepitia mateso mengi.
Amesema miradi mingi ya viongozi wasiounga mkono Chama Cha KUP haijalipwa hadi sasa.
Wakati uo huo Ozil amesema hakujakuwa na amani katika Bunge la Kaunti ya Pokot Magharibi tangu Gavana Lonyangapuo alipochukua hatamu ya uongozi.
Ametaja mabadiliko ya uongozi bungeni pamoja na kufurushwa kwa Spika Catherine Mukenyang’ mara kwa mara kuwa miongoni mwa masaibu ambayo Kaunti ya Pokot Magharibi imevumilia katika uongozi wa Lonyangapuo.
Ozili ameendelea kumpigia debe Simon Kachapin huku akielezea matumaini ya kuwapo kwa mabadiliko katika uongozi wa Kaunti hii iwapo atachukua uongozi.