VIONGOZI WA UDA POKOT MAGHARIBI WAPONGEZA HATUA YA KUAHIRISHWA UCHAGUZI WA CHAMA MASHINANI.

Viongozi wa chama cha UDA kaunti ya Pokot magharibi wameunga mkono hatua ya kuahirishwa uchaguzi wa mashinani wa chama hicho ambao ulikuwa umeratibiwa kuandaliwa tarehe 9 mwezi desemba hadi mwezi machi mwaka ujao.

Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walisema kwamba hatua hiyo itawapa wale ambao walikuwa wamefungiwa nje baada ya zoezi la kujisajili kukamilika rasmi jumamosi, nafasi ya kujisajili na kuwania viti mbali mbali vya chama hicho.

“Tunaunga mkono hatua ya kuahirisha uchaguzi wa mashinani wa chama chetu cha UDA. Hatua hii ambayo imechukuliwa na uongozi wa chama ni muhimu kwa sababu itawapa nafasi wale ambao hawakuwa wamejisali kuwania nyadhifa mbali mbali kufanya hivyo.” Alisema Lochakapong

Aidha Lochakapong alisema kwamba hatua hiyo ilifaa ikizingatiwa hali ya anga ya sasa ambapo maeneo mengi nchini yanashuhudia kiwango kikubwa cha mvua, hali ambayo huenda ingepelekea kushuhudiwa changamoto katika kuandaa uchaguzi huo.

“Kuna maeneo mengi nchini ambayo yanaendelea kushuhudia kiwango kikubwa cha mvua, na huenda hii ingekuwa changamoto kwa shughuli ya uchaguzi kuendelea. Kwa hivyo kuahirishwa uchaguzi huu kunatupa pia nafasi ya kujiandaa vyema kuufanikisha.” Alisema.

 Lochakapong alitumia fursa hiyo kuwakaribisha chamani wanachama wapya wanaojiunga na chama hicho cha UDA, na  kuwataka kuwa watulivu na kutovuruga chama anachosema kwamba kinashuhudia umoja wa wanachama wote.