VIONGOZI WA POKOT YA KATI WASHINIKIZA MAENDELEO KAMA NJIA MOJA YA KUKABILI UTOVU WA USALAMA.

Na Benson Aswani.

Mbunge wa sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo hasa wanaoishi maeneo ya mipakani na kaunti ya Turkana kujitenga na uhalifu na kuishi kwa amani.

Akizungumza jumatano baada ya mkutano wa amani uliondaliwa eneo la Lotong’ot, Lochakapong alielezea mipango ya kuchimba maji kwa ajili ya wakazi ili kukabili ukame ambao umetajwa kuwa chanzo cha mizozo ya muda mrefu miongoni mwa wakazi ambao wengi wao ni wafugaji.

“Tutachimba maji eneo hili ili wakazi watumie, kwa sababu mara nyingi ni tatizo la maji na lishe kwa mifugo ambayo husababisha hali ya utovu wa usalama. Na kwa kuwa tunatekeleza miradi hiyo, nawaomba sasa wakazi kuishi kwa amani.” Alisema Lochakapong

Aidha Lochakapong ambaye alikuwa ameandana na wakuu wa usalama katika mkutano huo aliwataka maafisa wa usalama kuwatafuta wahalifu wachache miongoni mwa jamii zote mbili na kuwakabili ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani.

“Hata baada ya kutafuta amani miongoni mwa jamii hizi zinazopakana kuna watu wawili au watatu ambao wanapotoka na kwenda kuwaua watu. Hawa ni watu ambao wanafaa kutafutwa na kukabiliwa kisheria. Lakini wakazi waendelee tu kuishi kwa pamoja jinsi imekuwa awali.” Alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wadi ya Masol Wilson Chekeruk alisema uhamasisho ambao umekuwa ukiendelezwa miongoni mwa wakazi, umepelekea kupungua kwa uhalifu, huku akitaka serikali kutekeleza miradi ya maendeleo eneo hilo swala alilolitaja kuwa suluhu kwa utovu wa usalama.

“Kumekuwepo na uhasama kati ya jamii ya Pokot na Turkana kwa muda sasa lakini uhamasisho ambao tumekuwa tukitoa kwa wananchi kuhusu haja ya kuishi kwa amani umesaidia kupunguza uhasama huo. Lakini kitu ambacho kinahitajika hapa sana ni kwa serikali kutekeleza miradi ya maendeleo.” Alisema Chekeruk.