VIONGOZI WA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VITENGO VYA USALAMA KUKABILI UHALIFU.

Kamishina kaunti ya Pokot magharibi Apolo Okelo ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana kushirikiana na idara za usalama katika kukabili hali ya utovu wa usalama katika mipaka ya kaunti hizo.

Akizungumza siku moja tu baada ya baadhi ya viongozi katika kaunti hizi mbili kulaumiana kuhusu hali ya usalama katika mpaka wa kainuk pamoja na mzozo unaohusu ujenzi wa kituo cha polisi eneo la lami nyeusi, Apolo aliwataka viongozi kuunga mkono juhudi za kuhakikisha kwamba usalama wa wananchi unaimarishwa.

“Nawasihi sana viongozi wa kisiasa kaunti ya Pokot Magharibi na Turkana kwamba tufanye kazi kwa pamoja katika kukabili changamoto ya usalama. Badala ya kupinga jambo ambalo litakuwa la manufaa kwa watu wetu, wacha tuunge mkono mradi huo kwani ndio suluhu kwa tatizo la usalama eneo hili.” Alisema Apolo.

Apolo alisema kwamba vitengo vya usalama havihusiani kwa vyovyote na maswala ya mipaka ila jukumu lake ni kuhakikisha wananchi kutoka pande zote mbili wanaishi kwa umoja na kuhakikishiwa usalama wao.

“Watu wanafaa kufahamu kwamba vitengo vya usalama havihusiani kwa vyovyote na mipaka. Kazi yetu ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa umoja na amani. Kwa hivyo ni ombi langu kwamba tusiingize mambo ya usalama kwa maswala ya mipaka.” Alisema.

Akizungumza wakati akizindua basary katika bustani ya Moi mjini Lodwar jumatatu, Gavana Lomurkai alinukuliwa akiwalaumu wakazi wa eneo la Kainuk kutoka kaunti ya Pokot Magharibi kuwa chanzo cha utovu wa usalama eneo hilo kwa kutaka kutwaa ardhi ya Turkana.

“Sisi tumeshindwa jirani zetu wanataka nini kwa kaunti yetu. Tumejaribu kuleta amani ila wao wanaharibu. Wako na ardhi yao, wako na kaunti yao lakini wanataka kuingia kwa kaunti yetu kwa lazima kuweka maendeleo yao.” Alisema Lomurkai.

Ni kauli ambayo ilijibiwa upesi na naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ambaye alisema ni jambo la kusikitisha kwa kiongozi wa hadhi ya gavana kutoa matamshi kama hayo aliyotaja kuwa ya uchochezi, na ambayo yanaweza kuibua uhasama miongoni mwa jamii hizi mbili ikizingatiwa utata unaokumba swala la ardhi.

“Inashangaza sana kuona mtu wa hadhi ya gavana kutoa matamshi kama haya ambayo yanaweza kuleta migawanyiko miongoni mwa jamii za Turkana na Pokot. Swala la ardhi ni nyeti sana na linahitaji mtu kuwa mwangalifu anapolizungumzia. Si kutoa maneno kiholela ambayo yanaweza kuzua vita.” Alisema Komole.

Alitoa wito kwa gavana huyo kuomba jamii ya Pokot msamaha kufuatia matamshi hayo, wakati uo huo akitoa wito kwa waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuendesha uchunguzi dhidi yake  na kumchukulia hatua.