VIONGOZI WA POKOT KUSINI WAMSHUTUMU MBUNGE WA ENEO HILO DAVID PKOSINGMbunge wa pokot kusini kaunti hii ya Pokot magharibi David Pkosing ameshutumiwa vikali kwa madai anayodaiwa kutoa katika vyombo vya habari kuwa naibu rais William Ruto alitoa fedha kwa baadhi ya viongozi alipozuru kaunti hii wiki iliyopita.
Mgombea kiti cha mwakilishi wadi ya Chepareria Teresa Lokichu amekashifu vikali madai hayo akimtaka Pkosing kuthibitisha madai yake kwa kutoa fedha hizo kwani yeye ni mmoja wa wabunge katika kaunti hii ambao anadai kuwa walikabidhiwa fedha hizo.
Aidha Lokichu ameshutuma kile amedai pkosing aliwalipa vijana wa boda boda kuandaa maandamano kudai fedha hizo akidai mbunge huyo alilenga kumharibia jina naibu rais, huku akiwataka vijana kutokubali kutumika kisiasa hasa wakati huu taifa linapokaribia uchaguzi mkuu.
Ni kauli ambayo imekaririwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Jackson Tutui ambao wamemtaka Pkosing kueleza ziliko fedha hizo, kwani matamshi yake yanaweza kuweka maisha ya viongozi wengine hatarini kwa kudhaniwa kukatalia fedha hizo.