VIONGOZI WA KUP WATOFAUTIANA KUHUSU HATIMA YA CHAMA HICHO KWENYE MRENGO WA AZIMIO.
Masaa machache tu baada ya kiongozi wa chama cha KUP aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo kutangaza kuondoa chama hicho katika muungano wa azimio la umoja, mbunge wa Pokot kusini David Pkosing amesema kwamba chama hicho hakijajiondoa katika muungano huo na kwamba kamwe hakiendi popote.
Katika taarifa, Pkosing ambaye ni naibu kinara wa chama hicho na ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, alisema kwamba taarifa ya Lonyangapuo ni maoni yake ya kibinafsi, na kwamba yuko huru kutoa maoni kulingana na misingi ya kidemokrasia ya chama.
“Chama cha KUP hakiondoki katika muungano wa azimio hivi karibuni. Yote ambayo aliyekuwa gavana alisema ni maoni yake ya binafsi na yuko huru kutoa maoni kulingana na demokrasia ya chama.” Alisema Pkosing.
Aidha Pkosing alisema kuwa anaunga mkono mkutano unaoandaliwa jumatano na muungano wa azimio akisema kwamba hauhusiani kivyovyote na mswala ya maandamano bali ni wa kuwahusisha wananchi katika kuiwajibisha serikali.
Alisema mikutano ya hadhara ni hitaji la kikatiba na hamna sheria yoyote ambayo imevunjwa na kinara wa azimio Raila Odinga katika kuandaa mkutano huo.
“Hamna mtu yeyote ambaye ameitisha maandamano. Kulingana na uelewa wangu kinara wa azimio Raila Odinga ameitisha mkutano wa kuuhusisha umma katika swala lililo na umuhimu mkubwa kwa taifa. Hayo si maandamano. Mimi binafsi naunga mkono mkutano huo.” Alisema.
Akitangaza jumanne kuondoa chama cha KUP katika muungano wa azimio, Lonyangapuo miongoni mwa maswala mengine aliutaja muungano huo kuwa hatari kwa usalama wa taifa, na kuwa chama cha KUP kamwe hakiwezi kushiriki katika mipango ya maandamano.
“Muungano wa azimio ni hatari kwa demokrasia, sheria na uwiano wa taifa. Hii leo tunaweka wazi kwamba chama cha KUP kinajitenga na maandamano ambayo yamepangwa na chama cha ODM kwa jina la muungano wa azimio. Swala hili halikujadiliwa na kukubalika na muungano wa azimio.” Alisema Lonyangapuo.