VIONGOZI WA KISIASA WALAUMIWA KWA KUKITHIRI UTOVU WA USALAMA MIPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA.

Mwakilishi wadi ya Seker Jane Mengich amewalaumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa hali ya utovu wa usalama ambayo imekuwa ikishuhudiwa mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana kwa muda sasa.

 Mengich alisema kwamba uvamizi wa mara kwa mara ambao unashuhudiwa maeneo ya mipakani pa kaunti hizi mbili umechochewa pakubwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao alisema wamekuwa wakitoa matamshi ya kiholela bila ya kujali matokeo yake.

Akizungumza katika hafla moja kwenye wadi yake, Mengich aidha alimhusisha kiongozi mmoja kutoka kaunti ya Turkana na mgogoro ulioshuhudiwa katika shule ya upili ya Turkwel ambapo wanafunzi wanadaiwa kukabiliana kwa misingi ya kikabila.

Alisuta vikali matamshi ambayo yalitolewa na kiongozi huyo wakati wa hafla ya kuadhimisha utamaduni wa jamii ya Turkana maarufu Tobonglore ambayo ilihudhuriwa na rais William Ruto.

“Viongozi wa siasa ndio wamechangia pakubwa utovu wa usalama mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na Turkana. Matamshi ambayo yalitolewa na kiongozi mmoja wa Turkana kudai kuwa sehemu kadhaa za kaunti hii ikiwemo Turkwel ni za Turkana ni ya kusikitisha. Ni matamshi kama haya ndiyo yaliyosababisha wanafunzi kutoka jamii ya Turkana kukabiliana na wenzao wa Pokot katika shule ya upili ya Turkwel.”  Alisema Mengich.

Mengich alisema inasikitisha kuona viongozi waliopewa jukumu la kuhakikisha usalama na huduma bora kwa wananchi ndio wanaozidisha mahangaiko ambayo wananchi wanapitia, akiwataka viongozi kudhibiti ndimi zao wanapokuwa katika mikutano ya umma.

“Viongozi wanapasa kuwa makini na maneno ambayo wanatoa katika mikutano ya umma. Kwa sababu sisi kama viongozi tumechaguliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi pamoja na huduma bora bali si kuchochea uhasama miongoni mwa wananchi.” Alisema.