VIONGOZI WA KISIASA WALAUMIWA KUFUATIA KUDORORA MAADILI MIONGONI MWA JAMII.


Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot Magharibi wamelaumiwa kutokana na kupotoka maadili miongoni mwa jamii hasa vijana.
Mwakilishi wadi ya Mnagei Richard Todosia alisema kwamba viongozi wa kisiasa ndio wamekuwa msitari wa mbele kupinga mikakati ambayo imekuwa ikiwekwa na wadau wengine ikiwemo machifu na viongozi wa kidini katika kukabili baadhi ya maovu kwenye jamii.
Todosia sasa ametoa wito kwa wadau mbali mbali kwenye kaunti hii ikiwemo wale wa kisiasa, usalama na wale wa kidini kushirikiana na kuzungumza lugha moja katika kuhakikisha kwamba jamii inazingatia maadili kwenye maswala mbali mbali.
“Mara nyingi mwanasiasa na kanisa hawaendi pamoja, mwanasiasa na chifu hawaendi pamoja. Na ni wanasiasa ndio wakaidi hapa kwa sababu chifu na kanisa wakisema bangi au pombe ni mbaya, sisi wanasiasa tunasema achia watu vitu vyao. Ukiangalia ni nani wananchi watafuata, si ni wanasiasa?” Alisema Todosia.
Aliendelea kwa kusema, “Tupo hapa kwa sababu ya kutozungumza kwa lugha moja. Ukiona watoto wanaharibika kimaadili ni kwa sababu hatutembei pamoja.”
Wakati uo huo Todosia alielezea haja ya vikao vya mara kwa mara baina ya viongozi na idara za usalama ili kupanga mikakati ya jinsi ya kuhakikisha usalama unadumishwa maeneo mbali mbali ya kaunti hii ya Pokot magharibi.
“Tufanye mkutano siku moja sisi wote na kuzungumze lugha moja. Hata wadau wote katika sekta ya usalama wanapasa kuandaa mikutano ya mara kwa mara ili kujadili mikakati ya kuimarisha usalama hii kaunti yetu.” Alisema.