VIONGOZI WA KISIASA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAISHAURI SERIKALI KUU KUWA NA UTU INAPOFANYA OPARESHENI KAPEDO


Viongozi kaunti hii ya pokot magharibi wameendelea kutoa wito kwa serikali kuwa na utu katika kuendeleza oparesheni ya kuwakabili wahalifu wanaosababisha ukosefu wa usalama eneo la Kapedo mpakani pa kaunti za Turkana na Baringo.
Wakiongozwa na seneta Samwel Poghisio, viongozi hao wametaka oparesheni hiyo kuendelezwa kwa kuzingatia haki za watoto na kina mama ambao anasema hawana uwezo wa kujilinda dhidi ya dhuluma zozote ambazo zinaweza kutekelezwa dhidi yao.
Aidha Poghisio ameishauri serikali kutafakari kuhusu njia mbadala za kumaliza visa vya mara kwa mara vya utovu wa usalama eneo hilo ambavyo husababishwa na wezi wa mifugo, ikiwemo kutilia mkazo swala la elimu miongoni mwa wakazi.
Ametoa wito kwa mashirika ya kijamii kuendeleza juhudi za kuwapelekea msaada wakazi wa eneo hilo ambao anasema wanakabiliwa na uhaba wa chakula na maji kutokana na ukame ambao unashuhudiwa.