VIONGOZI WA KIKE POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA KUTENGWA KISIASA.


Viongozi wanawake katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia kile wametaja kuendelea kutengwa licha ya kuwa wanapasa kuwa na viti zaidi katika chaguzi za humu nchini.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa mtandao wa Pokot Girl child network Teresa Lokichu, viongozi hao wamevitaka vyama vya kisiasa nchini kuzingatia sheria ya thuluthi tatu ya jinsia ili kuwapa nafasi zaidi wanawake kutoka kaunti hii kuwania nyadhafia za uongozi.
Lokichu amesema licha ya ugatuzi kutoa nafasi kwa wanawake kuongoza nyadhifa nyingi katika idara za serikali za kaunti, idadi ya wanawake serikalini ingali chini mno kutokana na baadhi ya tamaduni zisizotambua utawala wa wanawake.
Akizungumza katika kikao cha akina mama mjini Kapenguria, Lokichu amevitaka vyama vya kisiasa kutowabagua wanawake huku pia akitaka serikali kuwawezesha wanawake ili waweze kuwakilishwa vyema katika viwango vya wadi, kaunti na kitaifa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kundi la Setat Lilian Plapan amesema kuwa kina mama wako tayari kugombea viti vya kisiasa na kuungana mkono.
Aidha wametoa wito wa kuteremshwa viwango vya elimu kwa wanaogombea nyadhifa za kisiasa kwa wanawake wanaotoka jamii za wafugaji ambao hawakunafasika kupata elimu.