VIONGOZI WA KERIO VALLEY WAAHIDI KUSHIRIKIANA KATIKA KUIMARISHA USALAMA.


Mbunge wa Sigor katika kaunti hii ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ameahidi kushirikiana na viongozi wengine waliochaguliwa katika kaunti hii kuhakikisha kuwa kunapatikana amani mipakani pa kaunti hii na kaunti jirani za Baringo Elgeyo marakwet na Turkana.
Lochakapong amesema kuwa lengo lao kama viongozi wa kaunti hii na kanda nzima ya bonde la kerio ni kuhakikisha kuwa wakazi wa kaunti hizi wanaishi kwa amani na utangamano ili kuwezesha kuendelezwa shughuli muhimu za elimu na kibiashara zitakazopelekea maendeleo eneo hili.
“Jinsi Mungu ametupa nafasi hii, viongozi ambao wamechaguliwa tutashirikiana kuhakikisha kwamba amani inarejea tena kati yetu na jirani zetu ili soko zifunguliwe, shule zIrejelee shughuli zake ili maendeleo yaafikiwe kwa haraka.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong ameelezea imani kwamba serikali ya rais mteule William Ruto itaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kaunti za eneo la bonde la kerio zinapata maendeleo hasa ikizingatiwa zimesalia nyuma kwa kipindi kirefu kutokana na utovu wa usalama iwapo ushindi wake utadumishwa na mahakama ya juu.
“Tunafahamu kwamba hii serikali ya ‘hustler’ itaweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba sehemu hii ambayo iliachwa nyuma kwa muda mrefu inatengewa raslimali na fedha za serikali kuendeleza miradi ya maendeleo.” Alisema.