Viongozi wa kenya kwanza watetea michango wanayoendeleza maeneo mbali mbali ya nchi


Na Emmanuel Oyasi,

Viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi wanaoegemea mrengo wa rais William Ruto wamepongeza mtindo ambao umekumbatiwa na viongozi nchini wa kuendeleza michango ya kuyawezesha makundi ya akina mama na wahudumu wa boda boda nchini.


Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Prof. John Lonyangapuo, viongozi hao walisema hatua hii ni moja ya manifesto ya serikali ya kenya kwanza ya kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini.


Viongozi hao ambao walikuwa wakizungumza katika hafla moja eneo la Kacheliba, waliwataka kina mama na vijana katika kaunti hiyo kujiunga kwenye makundi na kuanzisha miradi ambayo itawapelekea kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi ili kuimarisha uchumi wao na kujiendeleza kimaisha.


“Hatua hii inaenda sambamba na mipango ya serikali ya kenya kwanza wakati tukitafuta kura kwamba tutakuja kuwasaida wakenya wa kipato cha chini ili nao waweze kujiwezesha kibiashara na kuimarisha uchumi wao,” alisema Lochakapong.


Wakati uo huo viongozi hao waliwashutumu viongozi wa upinzani ambao wanakosoa michango inayoendelezwa nchini kwa kuibua maswali kuhusu zinakotoka fedha hizo, wakisema kwamba ni viongozi wenye nia njema kwa wananchi ambao wamejitolea kuwasaidia kwa fedha zao wenyewe.


“Wale ambao wanakashifu michango hiyo hawana cha kuwapa wakenya. Pesa ambazo zinachangishwa zinatolewa na viongozi wenye nia njema kwa wakenya, ambao wamejitolea kwa fedha zao wenyewe kuhakikisha kwamba mkenya wa chini anawezeshwa,” alisema Lonyangapuo.