VIONGOZI WA KENYA KWANZA WAENDELEZA KAMPEINI KATIKA MAENEOBUNGE YA POKOT KUSINI NA KACHELIBA KAUNTI YA POKOT


Viongozi mbalimbali wa Muungano wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua wanatarajiwa kuzuru Kaunti ya Pokot Magharibi leo hii siku mbili kabla ya uchaguzi uliohairishwa ambao utafanyika siku ya Jumatatu.
Viongozi hao ni pamoja na Seneta wa Elgeiyo Marakwet Kipchumba Murkomen, Gavana wa Pokot Simon Kachapin, Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong’, Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto, Mbunge wa Kacheliba Mark Lomunokol na Senata wa Kaunti ya Pokot Magharibi Julius Murgor.
Viongozi hao ambao wanadaiwa kujigawa kwenye makundi mawili, wanatarajiwa kuyazuru Maeneobunge ya Pokot Kusini na Kacheliba kuwapigia debe wawaniaji wa ubunge kupitia kwa Chama Cha UDA.
Ikumbukwe kinyang’anyiro kikali kinashuhudiwa katika Eneobunge la Kacheliba baina ya Mbunge wa sasa Mark Lomunokol wa UDA na aliyekuwa naibu Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Titus Lotee kupitia kwa Chama Cha KUP.
Katika Eneobunge la Pokot Kusini kinyang’anyiro ni baina ya Mbunge wa sasa David Pkosing wa KUP, Simon Kalekem wa UDA na James Tekoo ambaye ni gombea huru.